Gavana Badilisha ataja ripoti kuhusu viazi kuwa ya kupotosha

Kulingana na ripoti hiyo, wakulima hutumia dawa nyingi za kuua wadudu kwa viazi wanavyokuza kwa ajili ya kuuza.

Marion Bosire and Lydia Mwangi
2 Min Read

Gavana wa kaunti ya Nyandarua, Moses Kiarie Badilisha, amepinga ripoti ya Chuo Kikuu cha Egerton kuhusu viazi vya kaunti hiyo, akiitaja kuwa tata, isiyo na msingi wowote wa kisayansi na ya kupotosha kabisa.

Gavana Badilisha alikosoa mbinu iliyotumika katika uchunguzi na matokeo ya ripoti hiyo yenye utata, akieleza kuwa ni jambo la kusikitisha kuwa suala nyeti kama hilo limeshughulikiwa bila kushirikisha wadau muhimu.

Anahisi wadau kutoka serikali na mashirika yasiyo ya serikali walistahili kuhusishwa akisema kuwa kutowahusisha kunatilia shaka uhalali wa ripoti hiyo, hasa katika suala la uthibitishaji.

Aidha, alitetea mbinu za kilimo za Kaunti ya Nyandarua, akisisitiza kuwa kaunti hiyo inashirikiana na Bodi ya Kudhibiti Dawa za Kupulizia (PCPB) ili kuhakikisha matumizi salama na ya kuwajibika ya dawa za kuua wadudu.

“Tumekuwa tukitoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wakulima wetu na kuhakikisha kwamba ni dawa zilizothibitishwa na kuidhinishwa pekee zinatumika. Juhudi kama hizi haziwezi kupuuzwa,” alisema.

Badilisha pia alitaja juhudi za kaunti katika kuzalisha mbegu za viazi zilizoidhinishwa na zisizo na magonjwa kama hatua muhimu ya kulinda afya ya walaji na ustawi wa wakulima.

Gavana alihimiza watafiti na taasisi nyingine zinazofanya kazi kama hizo kushirikiana na mamlaka za kaunti kabla ya kuchapisha ripoti ambazo zinaweza kudhuru, akisema ripoti kama hizo haziathiri tu taswira ya kaunti, bali pia huenda zikahujumu juhudi kubwa za wakulima.

Kaunti ya Nyandarua ni miongoni mwa zile ambazo huzalisha viazi kwa wingi nchini Kenya na imekuwa mstari wa mbele katika juhudi za kuimarisha na kuendeleza kilimo cha kisasa katika eneo hilo.

Website |  + posts
Share This Article