Samuel Mathu Wainaina ambaye ni mwakilishi wadi wa kaunti ya Nyandarua amewasilisha hoja ya kutaka kumbandua afisini Gavana wa kaunti hiyo Moses Kiarie Ndirangu maarufu kama Badilisha.
Hoja hiyo iliwasilishwa Novemba 11, 2024, na inaangazia makosa kadhaa anayolaumiwa kwayo Gavana Badilisha kama vile ukiukaji mkubwa wa katiba, utovu wa nidhamu katika masuala ya kifedha na matumizi mabaya ya mamlaka.
Akitaja kifungu nambari 181 cha katiba ya Kenya ya mwaka 2010, Wainaina alifafanua kwa kina kuhusu sababu za kutaka Gavana Badilisha abanduliwe madarakani.
Chini ya kosa la kukiuka katiba, Wainaina anamlaumu Gavana Kiarie kwa kuteua kinyume cha sheria washirika wake kusimamia ukusanyaji wa ushuru katika kaunti hiyo, na hivyo kudunisha mchakato wa ushindani wa kuajiri maafisa.
Gavana Kiarie analaumiwa pia kwa kile kinachotajwa kuwa kuamuru kufutwa kazi kinyume cha sheria kwa maafisa wa kaunti bila kufuata mpango ulio sawa kisheria.
Uajiri wa kiholela bila kufuata mipangilio pia umetajwa ukisemekana kusababisha uwepo wa wafanyakazi wengi kupita kiasi na hivyo kuongezea kaunti mzigo wa kulipa mishahara.
Kuhusu ufisadi na ukosefu wa maadili ya kifedha, Wainaina anasema Kiarie alitaka malipo yasiyo halali kutoka kwa wanakandarasi wa kaunti na wawasilishaji bidhaa katika kiwango cha asilimia 10.
Hatua hiyo kulingana na Wainaina imesababishia serikali ya kaunti ya Nyandarua madeni na bili nyingi ambazo hazijalipwa.
Chini ya kosa la tatu la matumizi mabaya ya mamlaka, Gavana huyo analaumiwa kwa kuelekeza malipo yasiyofaa kwa kampuni moja ya ujenzi anayohusishwa nayo, inayosemekana kufanya kazi duni katika mradi wa umma.
Wasemaji wa afisi ya Gavana Kiarie hata hivyo wanadai kwamba mjadala huo umechochewa na siasa wakisema amekuwa akitekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kwa maslahi ya kaunti nzima ya Nyandarua.
Iwapo hoja hiyo itakubaliwa badi kutakuwa na mjadala katika bunge la kaunti na iwapo utaungwa mkono na wanachama wengi wa bunge hilo, Kiarie ataondolewa afisini.