Gari walilokuwa wakisafiria maafisa wa KRA waliosombwa na maji Kwale lapatikana

Marion Bosire
1 Min Read

Gari ambalo maafisa wawili wa KRA walikuwa wakisafiria waliposombwa na maji ya mafuriko katika daraja la mto Ramisi, katika kaunti ya Kwale limepatikana.

Mkasa huo ulitokea Ijumaa Novemba 17, 2023 jioni wawili hao walipokuwa njiani kutoka LungaLunga kuelekea Mombasa.

Katibu wa usalama wa ndani Daktari Raymond Omollo amesema kupitia taarifa kwamba gari hilo aina ya Land cruiser limeopolewa na kubururwa hadi kituo cha polisi cha Msambweni.

Omollo ameelezea kwamba mikakati ya kutafuta miili ya wawili hao ambao wametambuliwa kama Joram Maina na David Ng’ang’a bado inaendelea.

Walioshuhudia kisa hicho walielezea kwamba wafanyakazi hao wa shirika la kukusanya ushuru nchini walipuuza ushauri wa kutovuka mto Ramisi uliokuwa umefurika.

Waendesha magari wengine walikuwa wameegesha magari yao karibu na daraja hilo kwa hofu ya kusombwa lakini wawili hao wakaendelea na safari.

Mratibu wa eneo la kusini katika shirika la KRA Lawrence Siele awali alielezea kwamba gari la wawili hao lilizidiwa na maji kwenye daraja hilo.

Aliahidi kuendeleza mawasiliano na familia za maafisa hao wawili huku akisisitiza kwamba usalama wa wafanyakazi wa shirika la KRA umepatiwa kipaumbele na wanafanya kila juhudi kuhakikisha miili yao inaopolewa.

Website |  + posts
Share This Article