Gari lililotumika kumteka nyara mwanablogu wa Meru Daniel Muthiani lapatikana

Tom Mathinji
1 Min Read
Gari lililotumika kumteka nyara Sniper lapatikana.

Maafisa wa polisi wa idara maswala ya upelelezi DCI, wamepata gari linaloaminika lilitumika kumteka nyara mwanablogu Daniel Muthiani Benard almaarufu Sniper.

Maafisa hao walisema uchunguzi uliofanywa umebainisha kuwa gari hilo pia lilitumika kuutupa mwili wa mwanablogu huyo katika mto Mutonga katika eneo la Chiakariga, kaunti ya Tharaka Nithi tarehe  mbili mwezi Disemba mwaka 2023.

Gari hilo aina ya Toyota Premio, lenye nambari za usajili KCR 742N, lilipatikana katika eneo la makazi la Canopy, eneo la Kithoka, kaunti ya Meru.

Kulingana na maafisa hao wa upelelezi, Vincent Mureithi Kirimi almaarufu Supuu, ndiye alikuwa akiliendesha gari hilo, alilolikodisha siku ambayo Sniper alitekwa nyara.

Brian Mwenda, Christus Manyara Kiambi na Boniface Kithinji Njihia maarufu DJ Kaboom, pia walisafirishwa kutumia gari hilo.

“Uchunguzi zaidi unaendelea, huku maafisa wa uchunguzi wa mauaji ya nyumbani wakijizatiti kukamilisha uchunguzi huo haraka iweekanavyo,” ilisema idara ya DCI.

Sniper alitoweka tarehe mbili mwezi Disemba mwaka 2023, huku mwili ake ukipatikana tarehe 16 mwezi huo katika mto Mutonga, kaunti ya Tharaka Nithi.

Uchunguzi wa maiti uliofanya na daktari Johansen Oduor, ulibainisha kuwa Sniper alifariki baada ya kunyongwa.

Uchunguzi huo pia ulidokeza kuwa mwili wa Sniper ulikuwa na majeraha kwenye mbavu na kichwa chake.

Share This Article