Gal Gadot asema alikuwa na damu iliyoganda kwenye ubongo akiwa mjamzito

Ametoa maelezo hayo kwenye Instagram akisema mwaka huu unaokaribia kuisha umekuwa wa changamoto nyingi mno maishani mwake.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwigizaji Gal Gadot alipitia wakati mgumu kiafya kabla ya kujifungua mwanawe wa nne akisema kwamba wakati huo alikuwa na damu iliyoganda kwenye ubongo.

Hali hiyo kulingana naye ililazimu afanyiwe upasuaji wa dharura ili kuokoa maisha yake.

Mwigizaji huyo alichapisha picha akiwa anamyonyesha binti yake wakiwa kwenye kitanda cha hospitali ambapo anaonekana mchovu kwenye Instagram.

Chini ya picha hiyo, Gadot alielezea madhila yaliyomfika kipindi hicho, akitaja mwaka huu kuwa wenye changamoto zaidi maishani mwake.

Amekiri kwamba amekuwa akipambana na fikra za kusimulia yaliyomfika au kunyamaza tu na akaamua kuachia moyo wake uamue.

Gal anasema mwezi februari akiwa ametimiza miezi minane ya ujauzito, alipatikana kuwa na damu iliyoganda kwenye ubongo.

Hii ni baada ya kusumbuliwa na maumivu makali ya kichwa kwa muda wa wiki kadhaa kabla ya kufanyiwa vipimo vya MRI kubaini tatizo.

Baada ya vipimo hivyo alikimbizwa hospitali na akafanyiwa upasuaji wa dharura saa chache tu baada ya kufika huko.

Anaelezea kwamba binti yake kwa jina Ori, alizaliwa wakati huo wa kutokuwa na uhakika na jina lake linalomaanisha ‘mwanga wangu’ halikuchaguliwa kimakosa.

“Kabla ya upasuaji nilimwambia Jaron kwamba binti yetu akiwasili, atakuwa mwanga unaonisubiri mwisho wa handaki hili.” ameandika Gadot.

Gal anasema alipata kupona kikamilifu na kuhimiza watu kuzingatia sana hali ya miili yao.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *