Wandani wa karibu wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua wamekashifu vikali kuongezeka kwa visa vya utekaji nyara nchini.
Wamezungumza haya wakati wa ibada ya mazishi ya watoto wanne walioteketea kutokana na mkasa wa moto wiki jana.
Ibada hiyo ilifanyika katika uwanja wa Gakoigo eneo bunge la Maragwa katika kaunti ya Murang’a.
Huku visa vya utekaji nyara vikiongezeka nchini, wandani wa Gachagua wamesema kuongezeka kwa visa hivyo kunatia hofu, na kwamba ni lazima serikali ichukue hatua dhidi ya vitendo hivi ambavyo vinahatarisha usalama wa Wakenya.
Viongozi hao, akiwemo Seneta wa Murang’a Joe Nyutu, wamehimiza maafisa wa serikali kuwachukulia hatua wale wanaokosea kupitia mfumo wa sheria badala ya kutumia utekaji nyara, wakiongeza kuwa vitendo vya utekaji ni kinyume cha sheria.
Gachagua amesisitiza kuwa wataendelea kukashifu vitendo hivi hadi vikome, akiongeza kuwa familia za waliotekwa nyara zinakabiliwa na hofu na majonzi.
Viongozi hao pia wamekiri kutotingizika kuunga mkono Gachagua katika mwelekeo wake wa kisiasa katika juhudi zake za kutetea haki na usalama wa raia, huku wakitafuta njia za kuboresha hali ya kisiasa nchini.
Taarifa ya Wambui Mwangi