Gachagua: Tuko tayari kushirikiana na jamii zote

Martin Mwanje
2 Min Read

Naibu Rais Rigathi Gachagua amesisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana na makundi mbalimbali kwa kusudi la kuhakikisha uwasilishaji wa ajenda ya serikali na kusikia moja kwa moja matarajio ya raia hasa vipaumbele vya kila kundi. Nia ni kuhakikisha ujumuishaji wa wote katika ajenda ya maendeleo ya serikali.

Gachagua ametoa wito kwa eneo la mashariki ya chini kuendeleza ajenda ya umoja wa eneo hilo na kukuza uhusiano mzuri wa utendakazi na serikali ili kupata huduma bora.

Akizugungumza wakati wa dhifa iliyoandaliwa na wanataaluma kutoka kaunti ya Kitui jana Jumatatu jioni, Gachagua alitoa wito kwa jamii ya Wakamba kuikumbatia serikali na kutokubali kutumiwa na wanasiasa kusababisha uharibufu. Alisema serikali iko tayari kufanya kazi na kila jamii.

Naibu Rais aliipongeza jamii ya Wakamba akiitaja kuwa jasiri na ambayo ina umoja unaopaswa kuigwa.

Waziri wa Utalii Peninah Malonza na Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Rais Dr. Monica Juma ni miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo iliyoandaliwa katika ukumbi wa Bomas of Kenya jijini Nairobi.

Lengo la hafla hiyo lilikuwa kuzungumzia ajenda ya maendeleo katika kaunti ya Kitui na eneo la mashariki ya chini.

Mazungumzo yaliangazia miradi muhimu inayopaswa kutekelezwa katika kaunti hiyo na njia bora za kutumia rasilimali zilizopo kuwanufaisha wakazi.

Wanataaluma waliwasilisha masuala mbalimbali yanayopaswa kuingiliwa kati na serikali ya kitaifa ili kuimarisha utoaji huduma.

Kadhalika uboreshaji wa barabara na upatikanaji wa maji safi ya kunywa na ya matumizi ya biashara ni miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa wakati wa mkutano huo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *