Naibu Rais Rigathi Gachagua anasema serikali inashirikiana na wabunge, magavana na viongozi wengine katika kuboresha taasisi za elimu ya juu ili kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Akiongea leo Jumamosi katika chuo cha mafunzo ya kiufundi cha Kipipiri, eneo bunge la Kipipiri, kaunti ya Nyandarua, Gachagua alitoa wito kwa wazazi kupea kipaumbele mafunzo ya kiufundi kwa watoto wao kwani elimu hiyo inatoa fursa zaidi za kujiajiri.
Aidha, alisema vyuo hivyo ni vichocheo vikuu vya kutoa ujuzi muhimu wa kujiajiri.
Gachagua alisema ni kupitia uwekezaji katika elimu ya kiufundi ndipo mahitaji ya maendeleo ya nchi yanaweza kuafikiwa.
Vilevile, aliwahimiza Wakenya kutambua ukweli kwamba vijana wanaofunzwa katika vyuo hivyo wana ujuzi wa kiufundi wa kubuni nafasi za ajira na kujitegemea.
Baadaye Gachagua alizuru shule ya upili ya wasichana ya Mawingo, alikoelezea kujitolea kwa serikali kuweka miundomsingi ili kupiga jeki mfumo wa mtaala wa CBC.
“Chini ya mtaala wa CBC, kuwiainisha miundomsingi ya kuafikia mahitaji yake ni lengo kuu la utawala wa serikali ya Kenya kwanza,”alisema Gachagua.