Naibu Rais Rigathi Gachagua, amewahimiza wakenya kuwa na subira, huku serikali ikijitahidi kuimarisha uchumi wa taifa hili.
Akizungumza mjini Nyahururu katika kaunti ya Laikipia siku ya Jumatatu, naibu huyo wa Rais alisema ajenda kuu ya Rais William Ruto ni kuboresha maisha ya wakenya wote kupitia miradi ya maendeleo.
Gachagua alimpongeza Rais Ruto kwa kuimarisha uchumi wa taifa hili tangu alipochukua uongozi wa nchi.
“Kwa mambo ya uchumi, Rais amejitahidi na matokeo yameanza kuonekana. Tulipoingia mbolea ilikuwa 7,000 na sasa ni 2,500. Unga ilikuwa 240 sasa ni 130, dollar ilikuwa 162 sasa ni 134, na ni kwa sababu ya mpangilio. Sasa kazi imeanza kuonekana,” alidokeza Gachagua.
Gachagua alisema jinsi alivyoagizwa na Rais, amehakikisha mipango ya serikali inatekelezwa kwa haraka, huku ikiafikia malengo yake.
Kuhusu vita dhidi ya pombe haramu na mihadarati, naibu huyo wa Rais aliwahakikishia wakazi wa kaunti ya Laikipia kuwa juhudi zake hazitatatizwa hadi janga hilo likabiliwe kikamilifu.
“Vita dhidi ya pombe haramu havitakoma. Viongozi wa serikali hapa wakiongozwa na kamishna wa kaunti, wanapaswa kuendeleza vita hivyo. Lazima tukabiliane na janga hilo ili tuwaokoe watu wetu,” alisema Gachagua.