Gachagua: Serikali haitalegeza kamba katika vita dhidi ya pombe haramu

Tom Mathinji
1 Min Read
Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ametoa wito kwa kundi la asasi mbali mbali za maafisa wa usalama, kukaza kamba katika vita dhidi ya pombe haramu na mihadarati.

Akiongea leo Jumamosi katika kaunti ya Meru, Gachagua alisema serikali haitalegea katika kuangamiza kabisa uovu huo, ambao alisema umezorotesha maadili ya kijamii hapa nchini.

“Rais Ruto, Waziri Kindiki pamoja na mimi, hatutakubali maisha ya vijana kuharibiwa na pombe haramu. Tumeweka mikakati mikali kuokoa kizazi hichi. Wale wanaouza pombe halali hawataguzwa,” alisema naibu huyo wa Rais.

Alisema serikali haiwezi kunyamaza watu wake wakifariki na wafanyibiashara wasiojali wakiendelea kujinufaisha kifedha.

Kuhusu sekta ya kilimo, naibu wa rais alielezea kujitolea kwake kulainisha sekta za kahawa na majani chai akisema kuwa marekebisho yanayotekelezwa katika sekta hiyo yameanza kuzaa matunda.

Naibu wa rais alisema kuwa serikali inapanga kufuta madeni yanayodaiwa vyama vya ushirika vya kahawa na itatoa tangazo kuhusu suala hilo, hivi karibuni.

Share This Article