Gachagua: Nitaendelea kutetea haki za wafanyabiashara

Tom Mathinji
1 Min Read
Naibu Rais Rigathi Gachagua azuru masoko ya Marikiti, Nyamakima na Gikomba Jijini Nairobi.

Naibu Rais Rigathi Gachagua amesema ataendelea kutetea haki za wafanyabiashara wadogo wadogo na ukuaji wa uchumi wa taifa hili.

Akizungumza leo Ijumaa alipowatembelea wafanyabiashara Jijini Nairobi, Gachagua alitoa wito kwa serikali ya kaunti ya Nairobi kubuni mazingira mwafaka ya biashara hususan kwa wale wanaofanya biashara ndogo ndogo.

“Nilipokea habari kwamba wafanyabiashara wanateseka na wanapinga baadhi ya sera zilizowekwa na serikali ya kaunti ya Nairobi. Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2022, mimi pamoja na Rais William Ruto tuliwaahidi wanabiashara kuwa hawatateseka tena. Tuliahidi mazingira bora ya kufanya biashara. Tunamuomba Gavana kutekeleza ahadi hiyo,” alisema Gachagua.

Gachagua aliyasema hayo alipozuru masoko ya Marikiti, Muthurwa, Gikomba na Nyamakima, kuzungumza na wanabiashara kuhusu maswala yanayokumba biashara zao na mazingira ya kazi.

Naibu huyo wa Rais alimtaka Gavana Sakaja kuwasikiliza washikadau kabla ya kutekeleza maamuzi ambayo huenda yakawakandamiza.

“Natoa wito kwa Gavana kuwashirikisha wadau kabla ya kutekeleza maamuzi,” alidokeza Gachagua.

Gachagua alikuwa ameandamana na wabunge kadhaa miongoni mwao James Gakuya (Embakasi Kaskazini), Benjamin Mejjadonk Gathiru (Embakasi ya Kati), Seneta wa Kiambu Karungo Thang’wa.

Wawakilishi wadi kadhaa pia walikuwepo wakiongozwa na mwakilishi wadi wa Nairobi mjini  Mwaniki Kwenya.

Share This Article