Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kinara wa chama cha DAP Eugene Wamalwa, na aliyekuwa Katibu Mkuu wa UDA Cleophas Malala, wametishia kuongoza maandamano ya kitaifa Januari mwaka ujao ikiwa visa vya utekaji nyara havitakoma.
Wakizungumza katika kijiji cha Makunga, eneo bunge la Navakholo, viongozi hao wametaka serikali kuwaachilia watu waliotekwa nyara na kuhakikisha usalama wa wananchi.
Rigathi Gachagua amewataka wananchi wa jamii ya Mulembe kuungana na kushirikiana na maeneo mengine kama Mlima Kenya ili kuwa na ushawishi mkubwa katika uongozi wa taifa siku zijazo.
Eugene Wamalwa na Cleophas Malala wamesema jamii ya Mulembe haitakubali kutumiwa kisiasa bila kunufaika, huku wakikosoa serikali kwa kushindwa kutekeleza ahadi zake kwa eneo hilo baada ya uchaguzi.
Viongozi hao pia wamekashifu mashambulizi na vitisho dhidi ya wale wanaonekana kushirikiana na Gachagua.
Wameapa kuendelea kupigania haki na kuhakikisha kwamba sauti za wananchi zinasikika kupitia hatua za kidemokrasia, ikiwemo maandamano ikiwa hali haitaimarika.