Naibu Rais Rigathi Gachagua amesema kuwa watumiaji bidhaa wanapaswa kufurahia bidhaa na huduma za ubora wa hali ya juu na usawa katika nyanja zote.
Kulingana na Gachagua, mataifa yana wajibu muhimu wa kutekeleza ili kuhakikisha masoko yanawavutia watumiaji bidhaa.
Ili kuafikia haya, alisema mikakati thabiti ya kisheria na ushirikiano sharti zibuniwe kati ya wahusika wa kitaifa na wale wa kimataifa.
Gachagua aliyasema hayo leo Jumatano alipofungua Kongamano la Kimataifa kuhusu Watumiaji Bidhaa la siku mbili lililoaza leo jijini Nairobi.
Kongamano hilo ambalo huandaliwa kila baada ya miaka minne, huwaleta pamoja watumiaji bidhaa, mashirika ya kijamii na wasomi kwa lengo la kutatua changamoto zilizopo pamoja na kuwakinga watumiaji bidhaa kote duniani.
Kulingana na waandalizi, kongamano hilo ni muhimu kwa wale ambao wamejitolea kuboresha maisha ya watumiaji bidhaa.