Naibu Rais Rigathi Gachagua amesifia makanisa akisema ni nguzo muhimu katika taifa la Kenya. Kulingana naye, makanisa yamechangia pakubwa hatua zilizopigwa na taifa katika ukuaji na maendeleo.
“Makanisa yamechochea sio tu utawala bora na kuanzisha taasisi za elimu, afya na nyingine ambazo zimeathiri kwa njia nzuri taifa hili la Kenya.
Kiongozi huyo aliahidi kwamba serikali itaunga mkono miradi ya makanisa na ya taasisi zilizoanzishwa na zinazoendeshwa na makanisa ili kuhakikisha zinaweza kujitegemea kifedha.
Alikuwa akizungumza katika kanisa la ACK St Francis Ciamanda huko Runyenjes, kaunti ya Embu, ambako alikwenda kuhudhuria ibada ya shukrani ya katibu wa mafunzo ya kiufundi Esther Mworia.
Naibu Rais alimsifia Mworia kwa kujitolea kwake kubadilisha elimu ya juu, bidii ambayo kulingana naye imeanza kuzaa matunda huku taasisi za mafunzo ya kiufundi zikipanuliwa kote nchini.
Lengo la upanuzi huo ni kuziba pengo lililopo katika maarifa na ujuzi vitu ambavyo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa la Kenya.
Viongozi waliokuwa wameandamana na Naibu Rais kwa ibada hiyo ya shukrani ni pamoja na mkuu wa utumishi wa umma Felix Koskei, Gavana wa kaunti ya Embu Cecily Mbarire, Seneta wa Embu Alex Mundigi, Seneta wa Nandi Samson Cherargei,wabunge Muchangi Karemba wa Runyenjes, Nebart Muriuki wa Mbeere Kusini, Mukunji Gitonga wa Manyatta na Geoffrey Ruku wa Mbeere Kaskazini kati ya wengine wengi.