Naibu wa Rais Rigathi Gachagua amevitaka viwanda vya majani chai viharakishe uwekezaji katika uzalishaji wa majani chai aina ya Orthodox, kwa sababu ya soko lake kubwa duniani.
Akisema majani chai hayo yana uwezo wa kukuza sekta hiyo na kuwaletea wakulima wa mashamba madogo madogo faida kubwa, Gachagua alivihimiza viwanda vinavyosimamiwa na halmashauri ya ustawishaji majani chai nchini, KTDA kupanua utayarishaji wa aina hiyo ya majani chai.
“Tunavihimiza viwanda vya majani chai kuangazia uzalishaji wa majani aina ya Orthodox sio tu ile ya black CTC. Viwanda hivyo vinapaswa kuimarisha uzalishaji wao kuambatana na majani chai aina ya Orthodox. Ina bei nzuri,” alisema Gachagua.
Naibu Rais aliyasema hayo wakati wa ibada ya Jumapili katika kanisa PEFA mjibi Thika.
Pia alitoa wito kwa wasimamizi wa viwanda vya KTDA kupunguza gharama za uendeshaji shughuli za viwanda hivyo kwa minajili ya kuongeza faida kwa wakulima wa mashamba madogo ya majani chai.
Kuhusu marekebisho katika sekta ya kahawa, Gachagua alisema pendekezo la marekebisho ya sheria ya kahawa, mswada wa kahawa wa mwaka 2023 ulio bungeni utaleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kahawa na akawahimiza wabunge kuupa kipoaumbele.