Naibu Rais Rigathi Gachagua anasema ataitisha mkutano wa viongozi kutoka Meru katika juhudi za kuwapatanisha Gavana Kawira Mwangaza na Wawakilishi Wadi wa kaunti hiyo.
Hii ni baada ya juhudi za Wawakilishi Wadi hao kumbandua mamlakani Gavana Mwangaza kugonga mwamba kwa mara ya pili.
Bunge la Seneti wiki iliyopita lilipuuzilia mbali mashtaka yote saba yaliyokuwa yamewasilishwa na Wawakilishi Wadi hao dhidi ya Gavana Mwangaza.
Gachagua anasema kwa mara nyingine, atajaribu kuzipatanisha pande hizo mbili baada ya majaribio yake ya awali kutofanikiwa.
“Meru kulikuwa na shida na masuala yaliyozozaniwa yamesuluhishwa na Seneti. Niliwataka viongozi hao kuridhiana lakini maridhiano hayo yaliduumu kwa kipindi cha mwaka mmoja pekee. Walianza tena kulumbana na tukajitenga nao. Nitaitisha mkutano wa viongozi hao utakaowahusisha Gavana, Wawakilishi Wadi na wabunge ili kuwaleta pamoja kwa sababu kaunti ya Meru pia ni muhimu sana kwa utawala wetu,” alisema Gachagua.
Akizungumza katika kaunti ya Embu, Naibu Rais alisema hatakata tamaa katika kutatua migogoro kati ya viongozi wa kaunti wanaozozana akiongeza kuwa ni wajibu wake kuhakikisha ugatuzi unafanya kazi.
Hayo yanajiri wakati mkazi mmoja wa kaunti hiyo amemtaka Rais William Ruto kuvunja serikali ya kaunti hiyo kufuatia mizozo ya mara kwa mara.