Naibu Rais Rigathi Gachagua atapewa jumla ya muda wa saa tano kujitetea atakapofika mbele ya bunge la Seneti Alhamisi wiki ijayo.
Kesi ya Gachagua itaanza kusikizwa na Seneti Jumatano ijayo, upande wa mashtaka ukitoa ushahidi wake.
Gachagua naye ametengewa Alhamisi kati ya saa tatu hadi saa saba adhuhuri kujitetea na kisha baadaye mawakili wake watoe ushahidi wao kwa saa moja kati ya saa nane unusu na saa tisa unusu.
Baadaye, bunge hilo chini ya uongozi wa Spika Amason Kingi litapiga kura kwa kila shtaka kati ya mashtaka 11 yaliyowasilishwa dhidi ya Naibu Rais.
Endapo Seneti itapitisha hoja hiyo kwa theluthi 2 ya Maseneta ambao idadi yao ni sawa na 44, basi Gachagua atatimuliwa afisini.
Hat hivyo, endapo Maseneta 23 watamuunga mkono Gachagua, hoja hiyo itaanguka na atasalia afisini.
Wabunge 282 walipiga kura ya kumbandua Naibu Rais wiki hii huku 44 pekee wakipinga hoja hiyo ya Mbunge wa Kibwezi West Eckomas Mwengi Mutuse.