Naibu Rais Rigathi Gachagua leo Ijumaa atahutubia Kamati ya Wakuu 10 wa Nchi na Serikali, C-10 ya Umoja wa Afrika, AU kuhusu kufanyiwa mabadiliko Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, UNSC jijini Ciudad de la Paz, Equatorial Guinea.
Gachagua atahutubia kamati hiyo kwa niaba ya Rais William Ruto.
Naibu Rais aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Obiang Nguema Mbasogo de Mongomeyen katika mkoa wa Djibloho jana Alhamisi jioni.
Alilakiwa na Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza Clementa Ngema na maafisa wengine serikalini, Naibu Mkuu wa Ubalozi wa Kenya mjini Addis Ababa nchini Ethiopia George Kwanya na kaimu kamishna mkuu mjini Abuja nchini Nigeria James Nyongesa miongoni mwa wengine.
Naibu Rais atahutubia mkutano wa wakuu wengine tisa wa serikali na nchi, wawakilishi wao, maafisa wa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya AU.
Hotuba yake, miongoni mwa masuala mengine, itaangazia ni kwa nini mabadiliko katika UNSC yanahitaji kuharakishwa kwa ajili ya uwakilishi sawa wa bara la Afrika kupitia upanuaji wa uanachama.
Kongamano hilo litafanyia mapitio ari inayochipuka ya kimataifa kuhusu haja ya kuifanyia UNSC mabadiliko ili kuiweka katika nafasi ya kimkakati na kuiandaa Afrika kwa matokeo yoyote katika mchakato huo ulioanza mnamo mwaka 2005.
Viongozi wa Nchi na Serikali kutoka nchi za C-10 pia watajadili namna ya kutumia kimkakati Nafasi ya Pamoja ya Afrika kama mpangokazi wa kufanya majadiliano ya kukubaliana juu ya mwelekeo halisi na madhubuti wa kuifanyia UNSC mabadiliko kwa ajili ya manufaa ya bara la Afrika.
Kamati ya Wakuu 10 wa Nchi na Serikali ya Umoja wa Afrika, C-10 ilianzishwa wakati wa kikao cha nne kisichokuwa cha kawaida cha umoja huo Agosti 4, 2005.