Naibu Rais Rigathi Gachagua, amewataka wanaokosa juhudi zake za kuleta umoja na usambazaji sawa wa rasilimali, kukoma kuhusisha juhudi hizo na ukabila.
Gachagua alisema uamuzi wake wa kushirikiana na upande wa upinzani katika eneo la Mlima Kenya, unalenga kuimarisha umoja wa kitaifa.
Naibu huyo wa Rais alisema juhudi hizo za kuhakikisha kuna ugavi sawa wa rasilimali kote nchini na kuunganisha eneo la mlima Kenya, zinalenaga kumpigia debe Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
“Ninapotoa wito wa umoja, watu hawapaswi kufananisha na ukabila. Tunataka tuwe na umoja kwa sababu tumejifunza kutokana na makosa ya migawanyiko ya hapo awali,” alisema Gachagua.
Akiwahutubia wananchi mjini Kagumo kaunti ya Kirinyaga leo Jumamosi, naibu huyo wa Rais aliwasuta viongozi wanaotilia shaka uaminifu wake kwa Rais William Ruto, akisema anafahamu vyema majukumu yake, na kwamba atahakikisha anatimiza wajibu wake kikatiba.
Aliyasema hayo baada ya kuhudhuria mpango wa kuwawezesha na kuwafadhili kimasomo mayatima katika kaunti ya Kirinyaga.
Mpango huo almaarufu ‘Tupange Kesho’ na ambao ulianzishwa na mwakilishi mwanamke wa Kirinyaga Njeri Maina, unalenga kufadhili elimu ya watoto kutoka jamaa maskini na mayatima.
Naibu huyo wa Rais alimpongeza mbunge huyo wa kaunti ya Kirinyaga, akitaja mpango huo kuwa wenye maono na utakaoleta mabadiliko.
Naibu huyo wa Rais alikuwa ameandamana na mbunge wa kaunti ya Kirinyaga Njeri Maina, Maseneta Kamau Murango na Samson Cherargei, mwenyekiti wa chama cha Jubilee Sabina Chege miongoni mwa viongozi wengine.