Naibu Rais Rigathi Gachagua ametoa wito kwa viongozi kukoma kupiga siasa za kumezea mate vyeo katika uchaguzi ujao na badala yake kuelekeza shabaha yao kwa shughuli zinazolenga kuboresha maisha ya raia.
Alitoa mfano wa shughuli hizo kuwa ufanyaji wa marekebisho katika sekta ya kilimo na uendelezaji wa miundombinu.
Akizungumza katika eneo la Githunguri, kaunti ya Kiambu leo Jumatano, Gachagua hasa alitoa wito kwa wabunge kutoa kipaumbele kwa upitishaji wa Mswada wa Vyama vya Ushirika.
Mswada huo unalenga kukuza nidhamu ya matumizi ya fedha katika vyama vya akiba na mikopo na kutoa mpangokazi unaohamasisha sekta endelevu na yenye ushindani ya vyama vya ushirika.
“Viongozi wanapaswa kukoma kupiga siasa na kutilia maanani kufanyia kazi marekebisho ya sekta ya kilimo na uendelezaji wa miundombinu,” alisema Naibu Rais.
“Tunapaswa kuungana kwa ajili ya maendeleo na kufanya kazi pamoja. Umoja ambao tumekuwa tukiitisha katika eneo hili la Mlima Kenya ni kwa ajili ya kushinikiza maslahi ya maendeleo. Tarehe ya uchaguzi ujao inajulikana, kwa hivyo kwa sasa hebu tuwafanyie kazi raia.”
Wakati huohuo, alisema marekebisho katika sekta za kahawa, majani chai na maziwa yanaendelea.
“Katika sekta za kahawa, majani chai na maziwa, tunapiga hatua nzuri na tunaelekea mahali. Suala letu tu ni uongozi wa vyama vya ushirika.”