Naibu Rais Rigathi Gachagua amewapongeza maafisa wa ununuzi, akisema wengi wao wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu na wanapaswa kuheshimiwa.
Akizungumza wakati wa mkutano wa pili kuhusu mchakato wa ununuzi na usambazaji katika kaunti ya Mombasa, Gachagua alitoa wito wa kutowashutumu maafisa wote wa ununuzi kwa ujumla.
“Kuna maafisa waadilifu katika sekta ya ununuzi na usambazaji. Kuna pia baadhi ya maafisa ambao hutekeleza ufisadi katika mchakato wa utoaji zabuni. Kuwakashifu maafisa wote kwa ujumla si haki, hatua hiyo inafaa kukomeshwa,” alisema Gachagua.
Hata hivyo naibu huyo wa Rais aliwataka maafisa hao wa ununuzi kukabiliana vilivyo na wenzao ambao wanaharibu sifa ya taaluma hiyo.
Huku akisikitika kuhusu ufisadi, ambao alisema unawanyima wakenya fursa ya kufanya biashara na serikali, Gachagua alitoa wito kwa asasi za uchunguzi kuwaajiri maafisa wa ununuzi na usambazaji bidhaa, ili kubabiliana na zimwi hilo la ufisadi.
“Natoa wito kwa asasi za uchunguzi kuwaajiri wataalam wa ununuzi kusaidia kuchunguza visa vya ufisadi. Baadhi ya maafisa wa polisi hawana ufahamu kuhusu swala la ununuzi,”aliongeza naibu huyo wa Rais.
Gachagua aliitaka tume ya maadili na kukabiliana na ufisadi EACC, kutia bidii zaidi katika kutokomeza ufisadi hapa nchini.