Naibu Rais Rigathi Gachagua ametaka vita dhidi ya pombe haramu kuimarishwa hata zaidi.
Akizungumza mjini Embu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Gachagua amelalamika kwamba ni wanawake ambao wamehisi mno makali ya athari za pombe haramu.
“Watu ambao wamehangaishwa na pombe, ile sumu, ile ya kuua watoto ni hawa wamama. Imekuwa vijana wamekunywa pombe ile mbaya. Wamelala kwa mitaro, maboma yameangamia, tmekosa watoto, tumekaa kama nchi imepotea,” alilalama Gachagua.
“Serikali wiki hii imetangaza mipango kabambe ya kuondoa sumu katika Jamhuri ya Kenya.”
Naibu Rais alirejelea agizo la kuvitaka viwanda vinavyotengeneza pombe haramu kufungwa kuwa baadhi ya mikakati ya kukabiliana na jinamizi la pombe haramu.
“Polisi wameagizwa kwamba wafunge viwanda visivyokuwa na leseni na kuharibu mitambo ya kutengeneza simu ya kuua watoto wetu,” aliongeza Gachagua.
Eneo la Mlima Kenya limeathiriwa mno na ubugiaji wa pombe haramu ambayo mara nyingi imesababisha maafa na nyakati nyingine kuvunja ndoa.
Serikali imeapa kufanya kila iwezalo kuhakikisha uzalishaji wa pombe haramu nchini unasitishwa.