Gachagua asema vita dhidi ya pombe haramu vinafanikiwa

Marion Bosire
2 Min Read

Naibu rais Rigathi Gachagua amesema kwamba vita dhidi ya pombe haramu na dawa za kulevya vimeanza kufanikiwa humu nchini.

Kiongozi huyo alisema kwamba serikali haitalegeza kamba katika oparesheni inayoendelea dhidi ya wanaouza pombe hiyo haramu kote nchini.

Gachagua ambaye alikuwa akizungumza jana kwenye hafla ya maombi ya kanisa la ACK dayosisi ya Mbeere alisema kwamba serikali imejitolea kukinga vijana wasidhuriwe na pombe haramu na dawa za kulevya.

Alisema kanisa linatakiwa kuchangia pakubwa katika ukuaji wa wa jamii katika nyanja mbali mbali ikiwemo kiuchumi kando na kuhimiza amani na umoja.

Naibu rais alizungumza pia kuhusu umuhimu wa umoja kati ya jamii za eneo zima la mlima Kenya akisema kwamba hakuna maendeleo ambayo yanaweza kuafikiwa bila umoja.

Alisisitiza kwamba jamii za eneo hilo huzungumza kwa lugha moja na hilo linapoendelea linachochea uwezo mkubwa katika ulingo wa siasa za kitaifa.

Ibada hiyo ya jana katika uwanja wa michezo wa Nyangwa iliongozwa na askofu mkuu wa kanisa la kianglikana nchini Daktari Jackson Ole Sapit.

Ilitumika pia kumsimika kwa mara nyingine Askofu Moses Masamba Nthukah kama askofu anayesimamia dayosisi na kusherehekea uteuzi wake kama mwamini wa kanisa la kianglikana nchini Kenya.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa eneo hilo akiwemo Gavana Cecily Mbarire.

Share This Article