Kulikuwa na mashaka baada ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kukosa kufika katika ukumbi wa Seneti wakati alipotakiwa kuanza kujitetea.
Gachagua alitarajiwa kuanza kujitetea majira ya saa 8:30 alasiri.
Hali hiyo ilimlazimu wakili mwandamizi Paul Muite kumuomba Spika Amason Kingi muda wa kwenda kubaini aliko mteja wake.
Subira subira hizo zilimfanya Seneta wa Kakamega Dkt. Boni Khalwale kumtaka Spika Kingi kuelezea mbona kanuni za bunge hilo zilikuwa zikikiukwa kufuatia kukosekana kwa Gachagua katika ukumbi wa bunge.
“Muda unayoyoma,” alilalama Dkt. Khalwale.
Hata hivyo, Spika Kingi alishikilia kuwa watamsubiri hadi Naibu Rais afikwe ukumbini kujitetea dhidi ya madai yake.
Spika Kingi alionya kuwa muda aliotengewa Naibu Rais hautaongezwa.
“Baada ya saa mbili, ikiwa Naibu Rais hatakuwa amefika ukumbini, nitatoa uamuzi wa kitakachofuata,” alisema Spika Kingi.
Wakati huo wote, Maseneta walitulia tuli kwenye viti vyao wakisubiri kuwasili kwa Naibu Rais anayekabiliwa na mashtaka ya kufurushwa madarakani.