Gachagua abadili nia, asema hawatasilisha lalama kwa JSC

Martin Mwanje
1 Min Read

Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa sasa hatawasilisha malalamishi yake kwa Tume ya Huduma za Majaji, JSC. 

Alikuwa ameapa leo Alhamisi kuwasilisha kwenye tume hiyo ombi la kutaka Jaji Esther Maina atimuliwe kwa namna alivyoshughulikia kesi ya ufisadi dhidi yake.

“Naibu Rais anafahamu mdahalo unaoendelea kwa sasa kuhusiana na uwazi katika idara ya mahakama na kifungu namba 10 cha katiba ya Kenya juu ya mienendo ya majaji na maafisa wa idara ya mahakama,” ilisema taarifa kutoka kwa Idara ya Mawasiliano ya Naibu Rais iliyotiwa saini na mkuu wake Njeri Rugene.

“Naibu Rais amepokea vyema taarifa ya Jaji Mkuu Martha Koome ya kutaka kufanyika majadiliano kuhusu suala muhimu la uwajibikaji katika idara ya mahakama, ambalo Rais William Ruto ameliunga mkono.”

Gachagua akongeza kuwa kwa misingi hiyo, hatawasilisha ombi lake mbele ya JSC kwa sasa.

Rais Ruto ameongoza shinikizo dhidi ya idara ya mahakama akiituhumu kwa kuzongwa na ufisadi anaosema umelemaza utekelezaji wa miradi ya serikali kama vile mpango wa nyumba za bei nafuu.

Jaji Koome ameashiria kuwa yuko tayari kukutana na Rais Ruto kuzungumzia masuala ibuka, wito ambao Ruto ameridhia.

 

Share This Article