Furifuri ya mashabiki uwanjani kwa mara ya kwanza tangu COVID 19, inapendeza

Dismas Otuke
2 Min Read

Mashabiki zaidi ya elfu 20 walifika uwanjani Nyayo jana kuishangilia timu ya Harambee Stars, ikichuana na Gabon katika mechi ya kundi F kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka ujao.

Kenya ilishindwa mabao 2-1 na wageni Gabon na kupoteza matumaini ya kufuzu kwa fainali za mwakani za Kombe la Dunia.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa mashabiki kujaa pomoni uwanjani kwa mechi tangu kusitishwa kwa mashabiki kuingia uwanjani miaka sita iliyopita wakati wa ugonjwa wa Covid-19.

Tiketi za jukwaa kuu zote zilikuwa zimeuzwa kufikia Jumamosi alasiri.

Katika kuonyesha hamu ya kurejea uwanjani kwa mara ya kwanza, mashabiki hao walipanga foleni ndefu kuanzia mapema jana kukaguliwa tiketi, kabla ya kuingia ndani ya uwanja.

Hata hivyo, baadhi yao walikosa subira na kuvunja mojawapo wa lango la kuingia Nyayo, hali iliyosababisha wengi wao kuingia hata bila tiketi.

Usalama wa hali ya juu ulidumishwa kutokana na pia ujio wa Rais William Ruto na viongozi wengine wa kisiasa waliofika uwanjani.

Serikali ilipiga marufuku mashabiki kuingia uwanjani mwaka 2020 kama tahadhari za kuzuia msambao wa COVID-19.

Mashabiki wamekuwa wakihudhuria mechi uwanjani, hususan za Ligi Kuu, Ligi ya NSL na mechi nyingine za fani mbalimbali za michezo tangu kuondolewa kwa vikwazo hivyo, lakini idadi ya jana ilikuwa kubwa zaidi kushuhudiwa kwa miaka sita iliyopita.

Mara ya mwisho ambapo mashabiki walifurika uwanjani kwa mechi ya Harambee Stars ilikuwa Septemba 8 mwaka 2018, wakati Kenya ilipowashinda Black Stars ya Ghana bao moja kwa bila na kufuzu kwa fainali za AFCON za mwaka 2019.

Hata hivyo, idadi ya mashabiki hao ilikuwa nusu uwanja sawia na idadi ya wale waliofika uwanjani jana.

Mashabiki kurejea uwanjani kwa mechi za soka au mashindano ni hatua ya kutia moyo na inayopaswa kupongezwa, kwani inachangia pakubwa kwa ukuaji wa mchezo.

Hatua hii inatia moyo zaidi huku Kenya ikiratibiwa kuandaa fainali za Kombe la CHAN Agosti mwaka huu kwa pamoja na Uganda na Tanzania.

Kenya itazialika Ushelisheli na Gambia mwezi Septemba mwaka huu katika mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia.

 

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *