Filamu ‘Barbie’ yapigwa marufuku Lebanon

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri wa Utamaduni nchini Lebanon alitangaza jana Jumatano kwamba filamu kwa jina “Barbie” haikubaliwi nchini humo na isionyeshwe kwenye kumbi za filamu kwa sababu inatetea ushoga na kukinzana na maadili ya kidini.

Mohammad Mortada anaungwa mkono na kundi la Waisilamu wa ki-Shia la Hezbollah, ambalo kiongozi wake Hassan Nasrallah, amekuwa akiendeleza harakati dhidi ya mashoga akisema ni hatari kubwa kwa Lebanon na wanafaa kukabiliwa.

Taarifa ya Waziri Mortada ilielezea kwamba filamu hiyo inapuuza umuhimu wa familia na akaielekeza afisi kuu ya usalama nchini Lebanon ambayo iko katika Wizara ya Mambo ya Ndani na ambayo imejukumiwa kutoa uamuzi wa udhibiti ichukue hatua za haraka kuhakikisha filamu hiyo haionyeshwi nchini humo.

Tukio hili ni kinaya ikitizamiwa kwamba Lebanon ndiyo ilikuwa nchi ya kwanza ya waarabu kukubalia maandalizi ya gwaride la mashoga mwaka 2017 na imechukuliwa kuwa makao salama kwa mashoga katika eneo zima la mashariki ya kati.

Lakini katika siku za hivi maajuzi, suala hilo limezua gumzo nchini Lebanon ambapo Waziri wa Mambo ya Ndani Bassam Mawlawi alitangaza marufuku dhidi ya hafla zote za kutangaza dhana potovu kingono, tangazo lake likichukuliwa kama linalolenga mashoga.

Bassam hajatoa maoni kuhusu kupigwa marufuku kwa Barbie.

Filamu hiyo imefikisha dola bilioni moja na zaidi katika mauzo ya tiketi tangu ilipozinduliwa Julai 21, 2023.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *