Fik Gaza afikishwa mahakamani Makindye, Kampala

Msanii huyo alikamatwa Alhamisi wiki iliyopita baada ya polisi kutekeleza msako nyumbani kwake.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda Shafiq Jjingo maarufu kama Fik Gaza aliyekamatwa na maafisa wa polisi Alhamisi iliyopita amefikishwa mahakamani leo katika eneo la Makindye, jijini Kampala, nchini Uganda.

Msanii huyo amekuwa katika korokoro za polisi katika kituo cha polisi cha Katwe kutokana na kile kilichotajwa awali kuwa makosa ya wizi wa kimabavu.

Baadaye jana, afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma nchini Uganda ilifanya mabadiliko katika makosa yake na kuyafanya kuwa wizi wa kawaida tu.

Sasa ripoti zinaashiria kwamba amepatikana na hatia mahakamani leo.

Maafisa wa polisi walitekeleza msako nyumbani kwa msanii huyo katika eneo la Makindye alhamisi wiki jana na wakamkamata pamoja na wenzake.

Msemaji wa polisi katika eneo la jiji la Kampala Patrick Onyango, awali alikuwa ameelezea kwamba hatua ya kuchelewa kufikisha msanii huyo mahakamani na wenzake hakuwa kwa nia mbaya.

Onyango aliitaja kuwa hatua iliyohitajika ya kuhakiki mchakato kufuatia mabadiliko katika mashtaka dhidi yake lakini hakutaja alichoiba na aliyemwibia.

Kupitia mitandao ya kijamii, msanii Fik Gaza, alikanusha madai dhidi yake akitaja kukamatwa kwake kama hatua ya kumharibia jina na hivyo kuhujumu kazi yake.

Website |  + posts
Share This Article