Familia moja huko Juja, kaunti ya Kiambu imeghubikwa na mateso na uchungu mwingi kufuatia kutoweka kwa mwanao wa umri wa miaka 14 kwa miezi miwili unusu sasa.
Daisy Wanjiku mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya upili ya wasichana ya Kahuhia katika kaunti ya Murang’a alitoweka nyumbani kwao mtaa wa Mugutha Mei 13, 2024 siku moja kabla ya siku ya kurejea shuleni kwa muhula wa pili.
Tangu wakati huo mamake msichana huyo kwa jina Julia Wairimu Githaiga hajakuwa na amani huku akimsaka mwanawe kila mahali bila mafankio na bila usaidizi wa maafisa wa polisi.
Mama huyo wa watoto wanne alielezea wanahabari kwamba Daisy ambaye ni mwanawe wa pili alitoka nyumbani saa mbili unusu usiku na hawajui aliko hadi leo.
Baada ya kumsaka kwa siku moja nzima bila mafanikio, Julia alipiga ripoti polisi washukiwa watatu wakakamatwa na kuachiliwa tena huku uchunguzi ukiendelea.
Bi. Githaiga ni mwingi wa imani kwamba atampata mwanawe akisisitiza kwamba maafisa wa polisi hawajampa usaidizi anaohitaji ili ampate.