Familia moja kaunti ya Kiambu yatafuta haki

Marion Bosire
1 Min Read

Familia moja mjini Thika katika kaunti ya Kiambu inatafuta haki baada ya mwanao kushambuliwa na afisa wa polisi kutokana na kile kinachosemekana kuwa kukosa kutoa hongo ya shilingi 100.

Martin Mwaura Mwangi wa umri wa makamo anaendesha kituo cha kufundisha mchezo wa kurusha vishale katika kijiji cha Komo ambapo alishambuliwa na afisa wa polisi aliyekuwa mlevi.

Afisa huyo anasemekana kutumia mkongojo wa Mwaura kumgonga kichwani kiasi cha kuanguka chini kisha akaendelea kumgonga kichwa na miguu hadi Mwaura akaanza kuvuja damu. Kwa sasa anauguza majeraha.

Mwaura anatumia mkongojo kutembea kutokana na maumivu aliyopata alipohusika kwenye ajali. Aliambia wanahabari kwamba wakati wa kisa hicho cha kushambuliwa na afisa wa polisi, alipoteza fahamu.

Inasemekana afisa huyo awali alikuwa amezuru kituo anachoendesha Mwaura akidai hongo kwa sababu hakikuwa kimesajiliwa inavyohitajika kisheria.

Kisa hicho kimesababisha ghadhabu kutoka kwa wakazi wa vijiji vya Githima na Komo ambao wanataka Mwaura apate haki kwani hakustahili unyama aliotendewa.

Kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Thika Andrew Sora amethibitisha kwamba maafisa wa polisi waliandikisha taarifa kutoka kwa wahusika wa kisa hicho pamoja na walioshuhudia.

Sora alisema uchunguzi unaendelea na iwapo afisa huyo wa polisi atapatikana na hatia, basi atafikishwa mahakamani.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *