Fahamu washindi wa FEASSSA 2024

Tom Mathinji
3 Min Read

Mashindano ya 21 baina ya shule za upili za Afrika Mashariki – FEASSSA, yalikamilika jumatatu mjini Mbale nchini Uganda huku shule mbalimbali kutoka mataifa shiriki yakinyakuwa mataji katika fani tofauti tofauti.

Tukianza na soka ya wavulana, waandalizi wa kipute hicho – Amus College walilipiza kisasi cha mwaka jana dhidi ya waganda wenzao waliopia mabingwa watetezi na washindi mara 14 wa taji hilo St. Mary’s Kitende kwa kuwalaza bao moja katika fainali iliyosakatwa chuoni Amus College.

Waakilishi wa Kenya – Musingu, waliibuka wa tatu walipowalemea waandalizi wengine Bukedea, magoli matatu kwa mawili.

Kwenye soka ya akina dada, wenyeji St. Noa waliwalemea Butere kwa bao moja lililofungwa kupitia mkwaju wa adhabu. Nyakach walimaliza wa tatu walipowakwatua Amus College kupitia matuta nane kwa saba baada ya sare ya magoli mawili kwa mawili.

Pili ni voliboli ya wavulana ambapo, Lycee Saint Luc de Nyabiharage (Burundi) walitawazwa mabingwa walipowazaba Bukedea CS seti tatu kwa moja.

Groupe Scolaire Officiel de Butare – GSOB ( RW) walikuwa wa tatu nao Cheptil wakimaliza wa nne. Upande wa wanadada, Kesogon ndio mabingwa wapya kufuatia ushindi wa seti tatu kwa nunge dhidi ya mabingwa wa taifa Kwanzanze.

Tatu, tuangazie mchezo wa vikapu vya wachezaji watano kila upande. Hapa, wenyeji Amus College, waliwapiku Laiser Hill alama 54 kwa 51.

ITS Gasogi (RW) walishika nafasi ya tatu. Vipusa wa St. Noa, Gs Marie Riene na St. Mary’s Kitende wote wa Uganda, walipata Dhahabu, fedha na shaba mtawalia.

Kwenye vikapu vya wachezaji watatu kila upande, FSK Kamusinga waliwazidi maarifa Seroma Christian (UG) viakapu 14 kwa 13 nao Amus College wakawa wa tatu.

Vile vile, vidosho wa Butere walileta taji hilo nchini kwa kuwazidi ujuzi St. Noa ( UG) vikapu 17 Kwa 15, nao St.Joseph wakaridhika na nafasi ya tatu. Daisy Awino wa Butere ndiye alitajwa mchezaji bora.

Mataji ya dhahabu, fedha na shaba ya mpira wa Pete yanamilikiwa na St.Mary,s Kitende, Mawanda SS na St.Noa za UG mtawalia.

Tukizamia Magongo,mabingwa wa taifa – Musingu ni wa kwanza kufuatia magoli mawili kwa yai dhidi ya St. Charles Lwanga nao Ntare (UG) ni wa tatu. Pia timu za Kenya za Wasichana – St.joseph , Nyamira na Tigoi zilinyakua uongozi kwa usanjari huo.

Mwisho ni darubini ya raga, ambapo kwenye wachezaji saba kila upande, Vihiga waliwabwaga mabingwa wa taifa – Bwake alama 26 kwa sufuri wakati Jinja SS ikimaliza ya tatu.

St.Joseph ndio bora kwa vipusa nazo Kinale (KE) na Nkoma ( UG) ni za pili na tatu mtawalia.

Katika Ile ya wachezaji 15 kila upande, mabingwa wa humu nchini, All saints Embu walinyakuwa ushindi wa alama tisa kwa tatu dhidi ya St.Mary’s Kisubi.

Makekere waliridhika na shaba. Kwenye fani hii, victor wawire wa Vihiga alitajwa mchezaji bora.

Wakenya pia walitamba katika mbio.

Makala ya 22 yataandaliwa nchini Kenya mjini Kakamega.

Share This Article