Baada ya maeneo yote manane kuandaa mashindano ya muhula wa kwanza baina ya shule za upili, hatimaye shule tofauti zimejikatia tiketi ya kuyawakilisha kwenye kindumbwendumbwe cha kitaifa kitakachoandaliwa katika chuo cha Shanzu, kaunti ya Mombasa kuanzia tarehe 5 hadi 12 mwezi ujao.
Katika raga ya wachezaji 15 kila upande kwa wavulana, mabingwa wa kitaifa na Afrika Mashariki All Saint’s Embu wa eneo la Mashariki wamerejea kutetea taji hilo.
Eneo la Magharibi litawakilishwa na wageni Vihiga (Vipers) sawia na Bwake wa Bonde la Ufa.
Nao Wavulana wa shule ya Kisii kutoka eneo la Nyanza wamerudi ulingoni kusaka taji hilo tena baada ya kuambulia patupu kwenye mashindano ya kitaifa ya mwaka jana kule Machakos.
Wenyeji (eneo la Pwani) watawakilishwa na timu mbili – Serani na Marafa, kwani eneo la Kaskazini Mashariki halina timu ya mchezo huo.
Timu zingine zilizofuzu ni Mang’u na Upper Hill za eneo la Kati na Nairobi mtawalia.
Kwenye Kitengo cha vipusa, mabingwa watetezi St. Joseph wa Bonde la Ufa wamo mbioni kutetea taji hilo huku Madira na Kinale kutoka Magharibi na eneo la Kati mtawalia wakiwa tayari kupinga.
Taji hilo pia linamezewa mate na Enkinda na St. Teresa za Nyanza na Mashariki mtawalia.
Katika fani ya mchezo wa magongo, miamba na mabingwa watetezi wa Afrika Mashariki na Kitaifa wa taji hilo – Musingu wa Magharibi wamo kwenye kundi B na Mpesa Foundation, Matiliku na Mnyenzeni za kutoka maeneo ya Kati, Mashariki na Pwani mtawalia.Hadi sasa, Musingu hawajafungwa bao tangu kuanza kwa mashindano ya mwaka huu.
Hata hivyo kundi A limebashiriwa na wengi kuwa balaa kwa sababu ya St. Antony ( Bonde la Ufa) na wenyeji St. Charles Lwanga waliomaliza wa pili na tatu kitaifa mwaka uliopita.
Wengine ni Hospital Hill – Nairobi na Ringa – Nyanza ambao pia ni moto kama pasi.
Upande wa vidosho, kundi A linajumuisha St. Charles Lwanga ( Pwani 1), AIC Nyayo ( Mashariki), na Mwiki ( Nairobi). Kundi B wamo mabingwa watetezi – Tigoi ( Magharibi), Ng’iya ( Nyanza), Kaloleni (Pwani 2) na Mpesa Foundation ( Kati).
Katika kipute hicho, wapenzi wa mchezo wa vikapu wa Pwani watashangilia wavulana wa Dr. Aggrey na kina dada wa Kaya Tiwi wa magharibi watashangilia Kamusinga na Butere, Mashariki watasimama nyuma ya Ghulamu wa Lukenya na vidosho wa Ikutha wakati Bonde la Ufa likiziba nyufa za barobaro wa Laiser Hill na mabinti wa St.Joseph.
Mashabiki wa Nyanza watatua kwa ajili ya wavuli wa Sawagongo na warembo wa Asumbi.
Pia Kuna mpira wa mikono ambapo mabingwa watetezi Kimilili na Moi Girls Kamusinga watapeperusha bendera ya Magharibi, Matiliku na warembo wa Kyeni watainua ya Mashariki, St.Albert Kamito na St. Joseph watabeba ya Bonde la Ufa, Manyatta na vipusa wa Kadika watalinda ya Nyanza, Makuyu na Wanamwali wa Thika watasafisha ya Kati nao waandalizi – Jaribuni na malkia wa Moi Forces Academy wang’arishe ile ya Pwani.
Zaidi ya hayo, wapenzi wa riadha watakuwa na kila sababu ya kutabasamu watakaposhuhudia wanariadha limbukeni wakitimuka kama risasi katika mbio fupi na ndefu.