Fahamu kuhusu Luanda Magere

Marion Bosire
5 Min Read

Viongozi wengi wa sasa na zamani wamesifika kwa matendo yao mazuri, mabaya au ya ajabu. Kauli hii imefanya vizazi vingi kuwasifu,kuwaiga au kuwakashifu. Baadhi yao waliacha maswali mengi ya jinsi walimudu mambo ya ajabu yasiyowai tokea kabla au baada yao. Kufuatia haya, jamii nyingi hasa za kiafrika hupajika watoto, barabara, majumba na hata taasisi majina ya watu hao kutegemea hali halisi. Hii leo, kwenye mwangaza wa wiki, tunaliangazia babe la kivita lenye sifa ya kutopenywa na silaha za kwa sababu alikuwa na mwili wa jiwe. Hali hii ilimwezesha kuongoza ukoo wa Sidho kushinda vita vingi dhidi ya mahasimu wao.

Lwanda Magere alizaliwa katika koo ya Sidho kwenye jamii pana ya Dholuo inayoishi kando ya ziwa Viktoria – Muhoroni na Nyando. inapakana na jamii ya Nandi kutoka kabila la Kalenjin na koo zingine za Dholuo. Kwa mujibu wa historia, Magere alizaliwa mwaka wa 1720. Baba na mama yake waliitwa Abonyo Awoud Omolo na Nyabera. Nyabera alifariki wakati akijifungua babe hili. Magere alipelekwa kwa bibiye aliyeitwa Rapondi kwa malezi hadi alipoufahamu ulimwengu kisha akarejea kwao. Abonyo naye aliiuwawa vitani na kumwacha Lwanda yatima ila alikuwa amebalehe.

Kwa mujibu wa jamii ya Dholuo, jina Lwanda lina maana ya jiwe kuu (Mwamba ). Nalo Magere limaanisha mzizi.

Sifa za gwiji huyu zilijiri nyakati zile alipoiongoza jamii yake kuwapiga na kuwanyanyasa maadui wao wa muda mrefu. Kabla ya ujio wake, Sidho waliuwawa kwa wingi na kunyanganywa mali yao.Aliposhika usukani wa jeshi la ukoo wake, walivuna ushindi mnono kwenye vita vyote walivyoshiriki dhidi Jo lang’o (Kalenjin).Hata walienda nyumbani kwa maadui hao na kuwanyanganya mali yao peupe,Jambo lililowapa furaha watu wa Sidho kwani walikuwa wameteseka kwa muda mrefu.

Hata hivyo, lililowashangaza watu wake na maadui ni jinsi alivyowauwa maadui wengi kuliko yeyote yule bila kujeruhiwa.Mishale, mikuki na silaha zingine za kivita hazikumpenya kwa vyovyote bali zake ziliwaingia maadui na kuwauwa kwa wingi. Kauli hii ilifanya maadui na watu wake kumwogopa zaidi. Ukoo wa Sidho waliona jambo hilo kuwa baraka kuu na kiboko cha Nandi.

Kadri siku zilivyosonga, ndivyo Magere alivyozidi kuimarika na kuwatokemeza mahasimu na Mali yao. Jamii ya Nandi walilemewa katika vita kiasi cha kumwacha afanye atekalo kwani mwenye nguvu mpishe.

Hata hivyo, palipo na wazee hapaharibiki jambo. wazee wa jamii ya Nandi walisuka njama ya kutegua babe hilo.Baada ya kuwaza na kuwazua, waliona heri kuiga ujuzi wa Wafilisti uliompoza Samson katika Bibilia. Walimzawadi Magere binti mrembo zaidi – Maryann, kama ishara ya amani baina ya jamii hizo. Wazee wa Sidho walimkanya kuridhia ndoa hiyo kwani huenda ilikuwa njama fiche, ila aliwapuuza licha ya kuwa na mke.

Maisha ya wachumba hao yalinoga na mara kadhaa Maryann alimuuliza jinsi alimiliki uwezo wa ajabu ila alikataa katakata kumwaga mtama.Hata hivyo, siku moja alipatwa na maradhi wakati mkewe mkuu hakuwepo. Alimweleza Maryann akate kivuliche na kutia dawa bila kujua anakuwa Samson aliyemweleza Delilah chanzo cha nguzu zilizomuuwa Simba na Wafilisti.

Maryann alistaajabu kuona kivuli kikitoa damu. Alitia dawa naye Magere akapona. Hapo akagundua siri ya dume hilo. Usiku ule, alitorokea kwao na kutegua kitendawili cha muda mrefu. Kwa kweli, lisemwalo lipo na kama halipo lii njiani laja kwani hatua ya Maryanne ilioana na kauli ya wazee wa Sidho kuwa huenda alikuwa kachero.

Baada ya kupata jawabu, jeshi la Nandi lilifanya shambulizi la kushtukiza lililosababisha maafa mengi.Wakati wa mapambano hayo, bado Magere aliwazidi nguvu na kuwafurusha. Ni katika harakati hizo ambapo mpiganaji mmoja wa Nandi alikumbuka siri waliyopewa na akarusha mkuki kwa kivuli cha Lwanda Magere.

Kifo cha Lwanda Magere kilikuwa pigo kuu kwa koo ya Sidho na jamii ya Dholuo kwa ujumla. Walihisi kama ndege ambao mti wao umekatwa.waliomboleza usiku na mchana ila kwa jamii ya Kalenjin ilikuwa hasira ya mkizi furaha kwa mvuvi.

Kwa sababu ya ukosefu wa teknologia maalum ya kunasa matukio wakati ule, simuli mbalimbali zinatofautiana kuhusu yaliyojiri baada ya kifo chake. Baadhi yazo zinaeleza kuwa aligeuka na akawa jiwe.Nyingine inaeleza kuwa, wakati wa mauti yake,mwili wake ulipotea, upepo wa kasi ukavuma eneo zima, wingu nzito likatanda na kiangazi kikakumba eneo hilo kwa miaka miwili. Baadaye, aliwajia wazee wawili kwa ndoto na kuwaeleze kuwa mwiliwe ulikuwa kando ya mto Nyando. Walipoupata mwili huo mvua kuu ilinyesha siku tatu kisha Wakaufanyia tambiko na mazishi ya heshima.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *