Evelyn Wanjiru ajitenga na madai ya mlahaka mbaya wa Nathaniel Bassey nchini Kenya

Wanjiru anasema iwapo Bassey alilakiwa visivyo kabla ya hapo hawezi kujua huku akikanusha madai ya video anayosema inasambazwa mitandaoni inayoelezea suala hilo.

Marion Bosire
2 Min Read
Nathaniel Bassey, Mhubiri Nigeria

Mwimbaji wa nyimbo za injili nchini Kenya Evelyn Wanjiru, amejitenga na madai ya mlahaka mbaya wa mhubiri na mwimbaji wa nyimbo za injili nchini Nigeria Nathaniel Bassey alipozuru Kenya.

Wanjiru, ambaye ni mwanzilishi wa mpango wa Praise Atmosphere, ametoa taarifa akifafanua kwamba kundi lake lilikuwa la pili kumleta Bassey nchini mwaka 2022.

Kulingana naye iwapo Bassey alilakiwa visivyo kabla ya hapo hawezi kujua huku akikanusha madai ya video anayosema inasambazwa mitandaoni inayoelezea suala hilo.

Katika video hiyo, Bassey ambaye anaoneka akuwa kwenye mahijiano anaelezea kwamba yeye huwa haitishi malipo anapoalikwa kuhudumu mahali, lakini anatarajia kwamba anapotumia kipaji chake kubariki watu nao wanatarajiwa kumbariki kwa njia nyingine.

Alielezea jinsi alialikwa nchini Kenya, akaja na kundi lake na baada ya huduma hakupata lolote akalazimika kugharamia usafiri na matumizi ya watu wa kundi lake katika hiyo safari.

Hata hivyo Bassey hajataja yeyote kuhusiana na madai hayo.

“Madai yanayoashiria kwamba mhubiri Bassey alidhulumiwa sio ya kweli” alisisitiza Wanjiru akiongeza kwamba Bassey alilakiwa na kuchukuliwa kwa njia stahiki alipoalikwa kwenye Praise Atmosphere.

Wanjiru amehimiza umma usikubali kuhadaiwa na taarifa zisizo za kweli akisema kwamba kundi la Praise Atmosphere na lile la Bassey yalichukua hatua kushughulikia suala hilo.

Mwimbaji huyo amehimiza umoja, upendo na maombi katika kanisa huku akiwahimiza kuangazia amri kuu ambayo ni kuliinua jina la Yesu.

Website |  + posts
Share This Article