Timu za Uholanzi na Uturuki zimefuzu katika robo fainali ya kipute cha bara Ulaya kinachoendelea nchini Ujerumani kufuatia ushindi wa magoli 3-0 na 2-1 dhidi ya Romania na Austria mtawalia.
Mabao hayo matatu hayo yalifungwa na Cody Gakpo dakika ya 20, kisha mchezaji wa akiba Donyell Malen akaongeza mawili dakika za 83 na 90+3.
Uturuki walifunga bao lao kupitia beki Merih Demiral mnamo dakika za 1 na 59, huku Michael Gregoritsch akiipa Austria la pekee dakika ya 66.
Kwenye robo fainali ya tarehe tano, Wenyeji Ujerumani watakabana koo na Uhispania saa moja usiku kisha Ureno imenyane na Ufaransa saa nne usiku.
Tarehe sita, Uingereza itakwaruzana na Uswizi saa moja usiku alafu Uholanzi na Uturuki ziumize nyasi saa nne usiku.