Washindi mara tano wa kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika,Toupiza Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na washindi mara nne ,Esperance kutoka Tunisia walijikatia tiketi kwa nusu fainali ya makala ya mwaka huu, baada ya kutwaa ushindi katika marudio ya robo fainali Jumamosi.
Mazembe wakicheza ugenini mjini Luanda, Angola walitoka nyuma na kusajili ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Petro Atletico, huku Esperance wakiilemea Asemc Mimosas ya Ivory Coast magoli 4-2 kupitia matuta ya penati kufuatia sare tasa .
Esperance watakabiliana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika semi fainali, huku Mazembe wakipimana ubabe na mabingwa mara 11 na mabingwa watetezi Al Ahly ya Misri .
Washindi baada ya mikumbo miwili ya nusu fainali watamenyana kwenye fainali, huku mabingwa wakituzwa dola milioni moja za Marekani na pia tiketi kushiriki kipute cha Kombe la Dunia mwaka ujao.