Mamlaka ya Kudhibiti Nishati nchini, EPRA imezindua kampeni ya ‘Tusonge na EVs’ inayolenga kuhamasisha umma kuhusu uhamaji wa umeme nchini na vilevile kukuza matumizi ya magari ya umeme (EVs).
Kampeni hiyo ilizinduliwa wakati wa hafla moja iliyofanyika jijini Nairobi na kushirikisha Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mtaifa (UNEP), Mpango wa Kimataifa wa Hali ya Hewa (IKI) na GiZ .
Waziri wa Nishati Davis Chirchir katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Mohamed Jabali alitaja uzinduzi huo kama hatua ya kufanikisha uhamaji wa umeme nchini Kenya.
Alitoa wito wa kuwepo kwa msimamo thabiti wa sekta ya umma na binafsi katika kukumbatia suluhu safi za usafirishaji kwa nia ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi kwa mazingira kwa asilimia 32 ifikapo mwaka 2030.
Chirchir aliongeza kuwa kanuni za uhamaji wa kielektroniki zinaendelezwa kwa kusudi la kuimarisha na kupanua mfumo wa udhibiti ambao tayari umewekwa, kuhakikisha kuwa ukuaji wa uhamaji wa umeme unasaidiwa na utawala mzuri na thabiti.