EPRA yatangaza bei zilizopunguzwa za mafuta

Marion Bosire
2 Min Read

Mamlaka ya kawi nchini EPRA imetangaza bei mpya za mafuta zilizopunguzwa na ambazo zitatumika kati ya Mei 15 na Juni 14 mwaka 2024.

Bei ya lita moja ya petroli imepungua kwa shilingi moja, ya dizeli ikapungua kwa shilingi moja na senti 20 huku mafuta taa yakipunguzwa bei kwa shilingi moja na senti 30.

EPRA imesema kwamba bei hizo mpya zinajumuisha ushuru wa asilimia 16 uliotangazwa na sheria ya fedha ya mwaka 2023.

Jijini Nairobi lita moja ya mafuta ya petroli itauzwa kwa shilingi 192 na senti 84, dizeli shilingi 179 na senti 18 na mafuta taa yauzwe shilingi 168 na senti 76.

Huko Kisumu bei ya Petroli, dizeli na mafuta taa itakuwa shilingi 192 na senti 66, shilingi 179 na senti 39 na shilingi 169 na senti moja mtawalia.

Mombasa Petroli itauzwa shilingi 189 na senti 66, dizeli shilingi 176 na senti moja na mafuta taa shilingi 165 na senti 59.

Punguzo la bei za mafuta mwezi huu ni la kiwango cha chini ikilinganishwa na mwezi Aprili ambapo bei hizo zilipungua kwa hadi shilingi 18.

Wakati huo lita moja ya petroli ilipunguzwa bei kwa shilingi 5 na senti 31, dizeli ikapunguzwa bei kwa shilingi 10 kwa kila lita na mafuta taa yakapunguzwa bei kwa shilingi 18 na senti 68.

Website |  + posts
Share This Article