Halmashauri ya kudhibiti sekta ya kawi na mafuta humu nchini (EPRA), inatarajiwa kutangaza bei mpya za mafuta siku ya Ijumaa, huku bei ya bidhaa hiyo ikitarajiwa kupanda.
Halmashauri hiyo, katika ilani kwa umma imeelezea kwamba itatangaza bei hizo kufuatia nyongeza ya asilimia 16 ya ushuru ziada wa thamani almaarufu (VAT) kwa bidhaa za mafuta kwa mujibu wa sheria mpya ya kifedha ya mwaka 2023.
Siku ya Jumatatu, Rais William Ruto alitia saini mswada huo kuwa sheria, hivyo kusababisha bei ya bidhaa za mafuta kuongezeka.
Kwa sasa bei ya lita moja ya Petroli Jijini Nairobi inauzwa shilingi Ksh182.4, mafuta ya Diesel shilingi 167.28 huku lita moja ya mafuta taa ikiuzwa shilingi 161.48.
Kulingana na Rais William Ruto, nyongeza ya asilimia 16 kwa bidhaa za mafuta kutasababisha ushindani na hivyo kuwavutia wawekezaji.