Kiongozi wa upinzani nchini Israel, Gadi Eisenkot, amemtaka Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuondoka madarakani.
Gadi anashtumu utawala wa Netanyahu kwa kutishia demokrasia kupitia madai ya kuingilia uchaguzi uliofanyika Oktoba 27.
Eisenkot alisema hayo jana Jumapili, muda mfupi baada ya wawakilishi wa pande hizo mbili za kisiasa kujadili uwezekano wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.
Katika taarifa, Eisenkot alisema Netanyahu na washirika wake wa karibu ni tishio la haraka kwa demokrasia ya Israel, akisisitiza kuwa hapaswi kuendelea kushikilia mamlaka.
Ukosoaji wake ulifuatia ripoti ya kituo cha televisheni cha Channel 12 iliyodai kuwa mkuu wa wafanyakazi wa Netanyahu, Ido Norden, alishawishi operesheni za polisi zilizowalenga wanachama wa chama cha United Arab List muda mfupi kabla ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wanachama watatu wa chama hicho walikamatwa kwa tuhuma za kuhusika na ununuzi wa kura baada ya polisi kupekua makazi yao bila hati za upekuzi.
Waliachiliwa baada ya wachunguzi kubaini kuwa taarifa za ujasusi zilizosababisha kukamatwa kwao hazikuwa na msingi.
Eisenkot ametaka uchunguzi wa haraka kuhusu madai hayo, akitaka polisi na shirika la ujasusi wa ndani la Israel, Shin Bet, kutoa maelezo.
Hakuna upande wowote wa kisiasa ambao umeweza kupata viti 61 vya bunge vinavyohitajika kuunda serikali.