Ebenyo aibuka kidedea Delhi Half Marathon

Dismas Otuke
1 Min Read

Mshindi wa nishani ya fedha ya dunia katika mbio za mita 10,000 Daniel Ebenyo Simiu, ametwaa ubingwa katika makala ya 18 ya mbio za Vedanta Delhi Half Marathon zilizoandaliwa Jumapili mjini New Delhi India.

Mbio hizo ziliwashirikisha Wakenya wanane ambao walikuwa kwenye kundi moja hadi umbali wa kilomita 13 ambapo Ebenyo na mwenzake Charles Matata, walichomoka na kuwaacha wengine na kisha baadaye Ebenyo akaongeza kasi na kukata utepe kwa dakika 59 na sekunde 27.

Matata alimaliza wa pili kwa dakika 60 na sekunde 5, huku Mhabeshi Addisu Gobena akiambulia nafasi ya tatu.

Bingwa wa Olimpiki mwaka 2016 Almaz Ayana kutoka Ethiopia, alishinda mbio za wanawake akiziparakasa kwa muda wa dakika 67 na sekunde 58 akifuatwa na Stella Chesang wa Uganda sekunde 28 baadaye, huku Viola Chepng’eno wa Kenya akikamilisha orodha ya tatu bora kwa dakika 69 na sekunde 9.

Share This Article