EACC, LSK zashirikiana kuimarisha vita dhidi ya ufisadi

Tom Mathinji
1 Min Read
Afisa mkuu Mtendaji wa EACC Abdi A. Mohamud na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Nchini (LSK) Charles Kanjama.

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) zimeshirikiana kuimarisha kwa pamoja vita dhidi ya zimwi la ufisadi.

Hayo yalitangazwa Jumatano baada ya mkutano wa mashauriano kati ya Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC Abdi Mohamud na mwenyekiti wa LSK Charles Kanjama, ambapo walikubaliana kutekeleza mageuzi muhimu ya kisheria ili kupiga jeki juhudi za kukabiliana na ufisadi.

Suala muhimu walilokubaliana kuangazia ni kuwahamasisha mawakili kuhusu jukumu lao la kuandaa ripoti chini ya sheria za mali inayopatikana kwa njia za uhalifu na ulanguzi wa fedha (POCAMLA).

Mpango huo unalenga kuimarisha jukumu la utaalam wa kisheria  katika kutambua, kutafuta na kutwaa mali iliyopatikana kwa njia haramu.

EACC ilielezea kujitolea kwake kushirikiana na LSK pamoja na washirika wengine katika sekta ya haki kupigia debe uwajibikaji, uadilifu na uongozi bora katika sekta ya umma.

Share This Article