EACC yarejesha ardhi ya mamilioni ya pesa iliyonyakuliwa mtaani Karen

Martin Mwanje
1 Min Read

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imerejesha ardhi yenye thamani ya mamilioni ya pesa iliyoko kwenye barabara ya Mukoma mtaani Karen, kaunti ya Nairobi. 

Ardhi hiyo inakadiriwa kuwa na thamani ya shilingi milioni 45 na inadaiwa kunyakuliwa na watu binafsi.

“Ardhi iliyorejeshwa yenye nambari ya usajili L.R. 2270/71 ambayo ukubwa wake ni hekta 0.029, ilisalimishwa kwa serikali ya Kenya mnamo mwaka 1994 kwa ajili ya ustawishaji wa vituo vya umma na ujenzi wa barabara ya umma,” ilisema EACC kwenye taarifa.

“Hata hivyo, miaka miwili baadaye, ardhi hiyo iligawiwa watu binafsi kinyume cha sheria.”

Katika uamuzi uliotolewa na Jaji Lucy Mbugua, mahakama ilibaini kuwa ardhi hiyo ni ya umma na kwamba uhamishaji wake kwa watu binafsi ulikuwa kinyume cha sheria, wenye udanganyifu na kifisadi.

Mahakama iliagiza kufutwa kwa hatimiliki ya ardhi hiyo na kuagiza kuwa isajiliwe kwa jina la serikali ya kaunti ya Nairobi kama ardhi ya umma.

EACC imepongeza hatua ya mahakama na kuahidi kufanya kila iwezalo kurejesha ardhi yote ya umma iliyonyakuliwa kwa njia ya kifisadi.

 

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *