Rais William Ruto anasema Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), zimejitolea kutekeleza maazimio ya mkutano wa pamoja uliofanyika mwezi uliopita Jijini Dar es Salaam, Tanzania, kuhusu mzozo unaoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Kulingana na kiongozi huyo wa taifa, lengo kuu ni kutatua mzozo unaoghubika DRC na kuleta amani ya kudumu.
Rais Ruto aliyasema hayo akiwa Jijini Windhoek, Namibia baada ya kushiriki mazungumzo na Rais wa Zimbwabe Emmerson Mnangagwa ambaye pia ni mwenyekiti wa SADC.
“Tulikubaliana kuendelea kushauriana na hatimaye kuandaa mkutano kati ya EAC na SADC juma lijalo, ili kujadili kwa mapana kuhusu mzozo wa DRC,” alisema Rais Ruto kupitia ukurasa wa X.
Wakati huo huo, Rais Ruto alisema alikubaliana na mwenzake wa Zimbabwe kuimarisha ushirikiano wa jumuiya hizo mbili ili kufanikisha makubaliano kuhusu eneo huru la kibiashara kati ya EAC,COMESA na SADC.
Rais Ruto alifanya ziara nchini Namibia kuhudhuria kuapishwa kwa Rais wa kwanza mwanamke wa Namibia Netumbo Nandi-Ndaitwah.