Waziri wa mazingira Aden Duale amesema kwamba mfumo elekezi wa kimkakati wa utunzaji mazingira katika sekta ya haki umejiri wakati mwafaka.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo huo, Duale alisema umejiri wakati ambapo ulimwengu unapambana na migogoro mitatu mikuu ambayo ni mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa viumbe hai na uchafuzi wa mazingira.
Alitaja mfumo huo kuwa hatua kubwa katika safari ya kitaifa ya kuhakikisha maendeleo endelevu na usimamizi mwafaka wa mazingira.
Duale alipongeza wahusika wote wa mfumo wa haki nchini chini ya baraza la utekelezaji wa haki nchini kwa mfumo huo ambao nia yake ni kuhakikisha mazingira bora siku za usoni.
Kulingana naye, mfumo huo ni jibu kwa wito wa kimataifa wa usimamizi bora wa mfumo ikolojia na unawiana na kujitolea kwa Kenya kuhakikisha uafikiaji wa malengo endelevu kufikia mwaka 2063.
Aliongeza kwamba ni jibu pia kwa malengo ya Kenya yaliyonakiliwa kwenye maono ya mwaka 2030 na mpango wa maendeleo wa Bottom Up kwa kuainisha mpangilio wa kutekeleza mipango ya uchumi wa kimazingira na uzuiaji wa mabadiliko ya tabianchi katika mfumo mzima wa haki nchini.
Waziri Duale alipongeza utekelezaji unaoendelea wa mikakati ya utunzaji mazingira katika mfumo wa haki nchini kama mabadiliko ya kijamii ya idara ya mahakama kupitia upatikanaji wa haki, kwa lengo la kuboresha utunzaji wa mazingira.
Alitaja pia mpango unaotekelezwa na idara ya magereza nchini wa utunzaji wa mazingira katika maeneo yaliyo karibu na vituo vya magereza kote nchini.
Mpango huo anasema umebadili baadhi ya wafungwa ambao sasa wamekuwa mabalozi wa utunzaji wa mazingira.
Matumizi ya magari machache na usimamizi unaofaa wa taka unaojumuisha kutumia tena taka na kilimo ni baadhi ya vitu ambavyo Duale alisema vitasaidia sana katika kutunza mazingira.