DRC yaanzisha mahakama ya makosa ya kifedha

Waziri wa Sheria Constant Mutamba ndiye alipendekeza mahakama hiyo ili kuimarisha mapambano dhidi ya ufisadi.

Marion Bosire
1 Min Read

Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC imeanzisha mahakama ya kushughulikia masuala yanayohusiana na uhalifu wa kifedha na kiuchumi nchini humo.

Haya yanafuatia hatua ya Rais Felix Tshisekedi ya kuidhinisha kuanzishwa kwa mahakama hiyo maalum.

Tshisekedi aliidhinisha pendekezo lililotolewa na Waziri wa Sheria Constant Mutamba la kuimarisha mapambano dhidi ya ufisadi nchini humo.

Kupitia amri maalum ya Rais, serikali imeanzisha Mahakama ya Jinai ya Kiuchumi na Fedha, chombo kipya cha kisheria, na jukumu lake ni kufuatilia na kusikiliza kesi za makosa makubwa ya kiuchumi.

Kwa mujibu wa mamlaka ya serikali, mahakama hiyo itashughulikia makosa kama vile rushwa, ubadhirifu wa fedha za umma, udanganyifu wa kodi na ukiukwaji wa sheria za forodha.

Duru za serikali zinaashiria kwamba mahakama hii imeundwa ili kuimarisha vita dhidi ya uhalifu wa kifedha na kuhakikisha wanaohusika katika ufisadi wanawajibishwa kisheria.

Mahakama hiyo itawekwa katika mji mkuu wa Kinshasa na itakuwa na afisi maalum ya mwendesha mashtaka. Itakuwa na uhuru wa kiutawala na bajeti yake binafsi.

Hatua hii inatazamiwa kama juhudi mpya za serikali ya DRC kuimarisha mfumo wa haki na kuongeza nguvu katika kupambana na uhalifu wa kifedha unaoathiri uchumi wa taifa.

Share This Article