Serikali ya Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo imewaita mabalozi wake nchini Kenya na Tanzania kwa kile kinachotajwa kuwa majadiliano.
Hatua hiyo ilitekelezwa Jumamosi Disemba 16, 2023 muda mfupi baada ya muungano wa kijeshi wa Congo unaojumuisha waasi kuzinduliwa jijini Nairobi.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje nchini Congo Alain Tshibanda, alitangaza hatua ya kuondolewa kwa mabalozi hao kupitia mtandao wa X.
Balozi wa Congo nchini Tanzania anasemekana kuitwa kwa sababu nchi hiyo ina makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC ambayo Congo ni mwanachama ikitizamiwa kwamba ilisitisha shughuli za kikosi cha pamoja cha EAC mashariki ya Congo.
Mwenzake wa Kenya anasemekana kuitwa na wizara hiyo ya mambo ya nje mjini Kinshasa kwa majadiliano.
Ijumaa, wanasiasa wakuu wa Congo na wawakilishi wa makundi kadhaa likiwemo lile la waasi la M23 ambao wameteka eneo kubwa Mashariki ya Congo, walizindua muungano kwa jina “Congo River Alliance” jijini Nairobi.
Kulingana na mmoja wa wahusika, muungano huo unaleta pamoja makundi kadhaa yaliyojihami ya Congo, makundi ya kijamii na ya kisiasa.
Corneille Nangaa, ambaye aliwahi kuhudumu kama msimamizi wa tume ya uchaguzi nchini Congo na ambaye aliwekewa vikwazo na Marekani kwa kuhujumu uchaguzi wa mwaka 2018 aliongoza uzinduzi huo.
Alisema lengo kuu ni kutafuta suluhisho la kudumu kuhakikisha watu wa Congo wanaishi pamoja kwa amani.
Haya yanajiri wakati ambapo Congo inajiandaa kwa uchaguzi wa Urais na wa wabunge Disemba 20, 2023.