Dkt Ronoh: Wakulima huchochea ukuaji wa uchumi nchini

Dr. Yusuf Muchelule
2 Min Read
Katibu katika wizara ya kilimo Dkt. Kiprono Ronoh amkabidhi mkulima miche ya kahawa, kaunti ya Kericho.

Katibu katika wizara ya Kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh, amesema kuwawezesha wakulima kuhakikisha wanapata pembejeo bora za kilimo, huchangia pakubwa katika kumarisha jamii na ujenzi wa taifa kwa jumla.

Dkt. Ronoh alidokeza kuwa hatua ya kuwawezesha wakulima, huboresha hali yao ya kiuchumi na kijamii na hivyo kukuza maendeleo.

“Kwa kuwapatia wakulima pembejeo bora za kilimo na fursa za kunawiri, wakulima watachangia pakubwa kwa ukuaji wa jamii yao na katika ujenzi wa taifa,” alisema Dkt. Ronoh.

Katibu huyo aliyasema hayo Ijumaa katika warsha ya kuwawezesha wakulima iliyoandaliwa katika eneo la Kipkelion Mashariki kaunti ya Kericho.

Katika hafla hiyo, Dkt Ronoh alitoa miche ya zao la kahawa kwa wakulima, kwa lengo la kuunga mkono juhudi za wakulima hao kuongeza uzalishaji.

“Zoezi hili linaashiria kujitolea kwetu kuwawezesha wakulima wa mashinani na kuchochea ukuaji wa uchumi katika sehemu za nyanjani,” alidokeza Dkt Ronoh.

Dkt. Ronoh alisema kupitia juhudi za pamoja na uongozi mwafaka, wizara yake inachukua hatua za kufanikisha ustawi na kuhakikisha utoshelevu wa chakula hapa nchini.

Katika hafla hiyo, Dkt. Ronoh aliandamana na mwakilishi wa kaunti ya Kericho Beatrice Kemei, mwenzake wa Bomet Linet Chepkorir mbunge wa eneo hilo Joseph Cherorot na waziri wa kilimo wa kaunti ya Kericho Magerer Langat, miongoni mwa wengine.

Dr. Yusuf Muchelule
+ posts
Share This Article