Serikali ya taifa kwa ushirikiano na serikali za kaunti, imezindua vituo vya kusambaza mbolea ya gharama nafuu kwa wakulima kote nchini.
Katibu katika wizara ya kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh, alisema hatua hiyo inawapunguzia wakulima mwendo mrefu na kuwaepusha kupanga foleni ndefu ili kupata bidhaa hiyo muhimu, hasaa wakati huu wa msimu wa upanzi.
Dkt. Ronoh alitoa wito kwa wakulima kupanda chakula kwa wingi, ili kuhakikisha utoshelevu wa chakula hapa nchini.
“Tuna bahati udongo wa eneo hili una rotuba ambayo inafanikisha ukuzaji wa aina mbali mbali za mimea. Tunapaswa kuchukua fursa hii kukuza chakula kingi na cha ziada,” alidokeza Dkt. Ronoh.

Katibu huyo aliyasema hayo Ijumaa, alipoongoza zoezi la usambazaji wa mbolea ya bei nafuu na mbegu zilizoidhinishwa, katika kaunti ndogo ya Kipkelion Mashariki, kaunti ya Kericho.
“Kilimo ndio uti wa mgongo wa taifa hili, kwani huhakikisha utoshelevu wa chakula. Ni muhimu kwamba uwekezaji katika sekta ya kilimo unapaswa kuhakikisha mazao yaliyoimarika,” alisema Dkt. Ronoh.
Alielezea kujitolea kwa serikali kuendelea kuwaunga mkono wakulima, ili kuboresha uzalishaji wa kilimo kwa lengo la kuhakikisha utoshelevu wa chakula na mapato kwa wakulima.