Dkt. Ronoh: Bei ya vyakula hapa nchini imepungua

Tom Mathinji
1 Min Read
Katibu katika wizara ya Kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh.

Katibu katika wizara ya kilimo Dkt. Kiprono Ronoh, amesema taifa hili limeshuhudia upungufu mkubwa wa bei ya vyakula.

Akizungumza katika mahojiano na shirika la utangazaji hapa nchini KBC, Dkt. Ronoh alisema utawala wa Rais William Ruto umejizatiti kuhakikisha wakenya wote wanapata chakula na kwa bei nafuu.

“Kuweka chakula mezani sio rahisi, lakini serikali imetia bidii kuhakikisha chakula kinapatikana na kwa bei nafuu,” alisema Dkt Ronoh.

Katibu huyo alitoa mfano ambapo alidokeza kuwa bei ya mfuko wa kilo mbili wa unga wa ugali imepungua, kutoka shilingi 250 hadi shilingi 103.

Na ili kuhakikisha serikali inazalisha mafuta ya kupikia chakula hapa nchini, Dkt. Ronoh alisema metrik tani 500 za mbegu ya alizeti, zimeagizwa na kusambazwa kwa wakulima katika kaunti 41.

Kulingana naye, alizeti hukuzwa katika maeneo ambako mahindi hukuzwa, na hivyo taifa hili lina uwezo wa kujinasua kutoka uagizaji mafuta ya kupikia, na kuanza uzalishaji wake hapa nchini.

“Huku tukiwa na takribani ekari milioni 44 ya ukuzaji mahindi, tuna fursa ya kutatua upungufu wa mafuta ya kupikia hapa nchini,” alisema Dkt Ronoh.

Website |  + posts
Share This Article